Home » » MWANAHARAKATI NA MWANDISHI WA KITABU CHA DIRA YA MAENDELEO MAYROSE MAJINGE TOKA DAR ES SALAAM ASHIRIKI KAMA MGENI MAALUM KATIKA ZOEZI LA UTOAJI TUZO KWA WAKULIMA SIKU YA NANENANE NZEGA TABORA

MWANAHARAKATI NA MWANDISHI WA KITABU CHA DIRA YA MAENDELEO MAYROSE MAJINGE TOKA DAR ES SALAAM ASHIRIKI KAMA MGENI MAALUM KATIKA ZOEZI LA UTOAJI TUZO KWA WAKULIMA SIKU YA NANENANE NZEGA TABORA





       Mwanaharakati na Mwandishi wa Vitabu Mayrose Majinge akizungumza na wananchi 
       wa Nzega siku ya sherehe za utoaji Tuzo kwa wakulima Wilayani Nzega siku ya nane 
      nane.

                  Dada Lilian Wasira Mwanasheria katika picha siku ya sherehe za utoaji Tuzo   
             kwa wakulima, wafugaji na taasisi zilizo saidia wakulima Wilaya ya Nzega Tabora

Na Protas Charle – IDN

Mwandishi wa kitabu cha Dira ya Maendeleo Mayrose Majinge na Mwanaharakati wa maendeleo nchini toka Jijini Dar-es-salaam, ashiriki katika zoezi la utoaji wa tuzo kwa wakulima katika sherehe za sikukuu ya wakulima Wilayani Nzega Mkoani Tabora.

Tukio hilo la utoaji wa tuzo kwa wakulima lililofanyika tarehe 8/8/2013 katika Ukumbi wa Channel One Nzega Mjini, liliandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya IDN kwa lengo la kuenzi wakulima na wafugaji wadogowadogo wa Wilaya ya Nzega ili kuonesha mchango wanaoutoa kwa jamii.

Akizungumza katika ufunguzi wa sherehe hiyo ya utoaji tuzo Mratibu wa IDN ndugu Boniphace Nyabweta alisema taasisi yake iliona ni vema kuandaa tuzo kwa wakulima na wafugaji ili kuwakumbuka kwani wakulima na wafugaji wamekuwa hawakumbukwi kwa mchango wanao utoa katika jamii hivyo kupitia tuzo hizo zitaleta hamasa kubwa kwa washindi kuwa na hamasa ya kuongeza bidii katika uzalishaji wa mazao yao.

Katika sherehe hizo taasisi ya IDN ilishirikisha wakulima, wafugaji na taasisi kama vile TASAF-Nzega, PRIDE-Nzega, SEDA-Nzega, BRAC-Nzega,na TECHNOSERVE zilizotoa mchango kwa namna mbalimbali kwa wakulima na wafugaji ambapo mchujo ulifanyika na kuwapata washindi kumi na tatu ambao walijinyakulia tuzo kila mmoja.

Miongoni mwa tuzo zilizo kuwa zikishindaniwa ni pamoja na tuzo ya Mkulima bora wa bustani, mkulima bora wa matunda, mkulima bora wa zao la chakula, mjasiriamali bora wa usindikaji wa mazao ya kilimo. Tuzo nyingine ni mfugaji bora wa kuku wa kienyeji, mfugaji bora wa kuku wa nyama, mfugaji bora wa kuku wa mayai, mfugaji bora wa nguruwe, mfugaji bora wa ngombe na mbuzi n.k

 Mapema kabla ya zoezi la utoaji tuzo kuanza Mayrose Majinge ambaye pia alikuwa mgeni maalum aliwasilisha mada kwa wageni iliyohusu maendeleo ya kilimo na maendeleo kwa vijana. Alisema katika dhana nzima ya maendeleo akilenga kijana kuwa, kijana ni mtu yeyote ambaye anajishughulisha kufanya kazi za maendeleo pasipo kujali umri.

Alieleza kuwa wapo wazee wengi wenye miaka zaidi ya sitini lakini wanafanya kazi sana hivyo kwa tafsiri ya kimaendeleo hao ni vijana. Pia wapo vijana wenye umri wa miaka ishirini nakadharika lakini wamekaakaa tu pasipo kufanya kazi, kwa tafsiri ya kimaendeleo hao si vijana.

Akizungumzia juu ya uongozi Mwanasheria Lilian Wasira aliyeambatana na Mayrose, alisema vijana wasikae na kulalamika vijiweni kwani wanapaswa kushiriki katika kuwania nafasi za kugombea kuwa viongozi katika Nyanja zote. “Katiba yetu inasema kila mtu anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi za uongozi, hivyo kila kijana anapaswa kugombea pale anapo hisi anaweza na sio kulalamikia uongozi uliopo madarakani, alisema.

Washindi kumi na tatu waliibuka na kupata tuzo ambapo waliomba zoezi hilo liendelee kila mwaka ili kuwahamasisha wakulima na wafugaji wa Wilaya ya Nzega kuendelea kujikita zaidi katika shughuli za kilimo na ufugaji.

Share this article :
 
Support : Swahiliclan | harold | 0752490120
Copyright © 2011. YOUTH FOR CHANGE - All Rights Reserved
Template Created by swahiliclan Published by hashork
Proudly powered by sc