Na: Protas Charle
Taasisi isiyo ya Kiserikali INFORMATION FOR
DISSEMINATION NETWORK (IDN) inayofanya kazi Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora,
kupitia mradi wa kuwezesha vijana kujiajiri YOUTH FOR CHANGE kupitia fursa ya
Kilimo na Teknolojia ya habari na mawasiliano, imeandaa tuzo kwa wakulima,
wafugaji na taasisi zilizosaidia wakulima wa Wilaya ya Nzega.
Tuzo hizo zitatolewa siku ya sikukuu ya wakulima
maarufu kama nanenane ambapo taasisi hiyo imeamua kuthamini mchango wa wakulima
wadogo wa Wilaya ya Nzega ili kuwapa hamasa ya kuendelea kujikita zaidi katika
kilimo cha biashara na kuondokana na kilimo cha mazao ya chakula pekee.
Akizungumza katika mahojiano na wanahabari wa taasisi
hiyo inayojishughulisha na usambazaji wa habari kwa jamii, Mratibu wa Mradi Ndugu
Boniphace Nyabweta, alisema taasisi yake kupitia mradi wa kuwezesha vijana
kujiajiri kupitia kilimo na teknolojia ya habari na mawasiliano wameamua
kuandaa Tuzo kwa lengo la kuwakutanisha wakulima, wafugaji na taasisi
zilizosaidia wakulima wa Wilaya ya Nzega katika kipindi cha mwaka 2012/2013.
Aidha, mratibu alisema kutokana na vijana walio katika
mradi wa Youth for Change, kutekeleza mradi wa Kilimo na Teknolojia ya habari
na mawasiliano, itasaidia wakulima wa Wilaya ya Nzega kujifunza mambo
mbalimbali yatakayo wasilishwa katika sherehe hizo za utoaji tuzo na kupata
taarifa za kilimo, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, masoko, mikopo na
kuwasilisha kero wanazozipata katika kazi zao kwa viongozi wa Serikali ili
zishughulikiwe.
Alisema mgeni rasmi katika utoaji wa tuzo hizo atakuwa
Afisa Kilimo wa Wilaya ambapo ataambatana na watendaji wengine toka katika
idara ya kilimo na mifugo wa halmashauri ya Nzega na viongozi wa idara ya
maendeleo ya jamii Wilaya.
Mratibu alibainisha baadhi ya Tuzo zitakazo tolewa ni,
Tuzo ya mkulima bora wa Bustani, Mkulima bora wa mazao ya biashara, mfugaji
bora wa kuku, mfugaji bora wa ng’ombe, mfugaji bora wa nguruwe n.k