Wednesday, July 10, 2013
BRELA yarahisisha huduma za usajili wa biashara na kampuni.
Wanahabari wakipitia nakala ya kitabu chenye taratibu za kusajili kampuni na biashara BRELA. |
Andrew Mkapa, Naibu msajili mkuu wa idara ya sheria za biashara BRELA akitoa ufafanuzi kwa wanahabari leo asubuhi. Kushoto kwake ni Kaimu meneja huduma, utawala na fedha BRELA, Bosco Gadi akimsikiliza kwa makini.
Wajasiriamali wadogo na wakubwa wameaswa kusajili biashara
zao na kupata kampuni zitakazowasaidia kufanya biashara kwa kushirikiana na
makampuni makubwa ya ndani na nje.
Hayo yamezungumzwa na kaimu meneja huduma, utawala na fedha
wa wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA), Bosco Gadi wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari MAELEZO
jijini Dar es Salaam leo asubuhi.
Bosco ameweka wazi kuwa ili kurahisisha ushawishi wa
kusajili biashara kwa wajasiriamali nchini, BRELA wameamua kushirikiana na
chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) ili
kuwasaidia kushawishi wajasiriamali kuanzia ngazi ya vijiji, wilaya na mikoa.
“Kuchaguliwa kwa TCCIA kumetokana na wao kuwa na mtandao mpana
wa kielektroniki unaounganisha ofisi zao wilayani takriban mikoa yote ya
Tanzania.
“Kupitia utaratibu huo, gharama za usajili wa jina la
biashara ni Sh 6,000 ambazo wateja hulipia na kupatiwa stakabadhi za BRELA na
TCCIA inatoza kiasi kidogo cha fedha Sh 2,000 kwa kila jina la biashara kwa
ajili ya huduma za kiutawala ikijimuisha gharama za utumaji wa maombi hayo
ofisi kuu ya BRELA,” alisema Bosco.
Aidha kwa upande wa usajili wa makampuni ada ya usajili
inayotakiwa kulipwa inategemeana na kiasi cha mtaji mteja anachoandika kwenye
katiba ya kampuni anayotarajia kuisajili. Gharama yake inaanzia Sh 50,000 kwa mtaji
unaoanzia Sh 20,000- Sh500,000, mteja atalipia Sh 300,000 kwa mtaji unaoanzia
Sh 30,000,000.
Katika hatua nyingine kaimu meneja huyo ameweka wazi kuwa
kwa sasa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia BRELA wanapokea maombi
ya kusajili biashara na kampuni kwa kutumia njia ya mtandao, mteja anatakiwa
kuingia kwenye tovuti ya BRELA ambayo ni www.brela-tz.org
na kuangalia orodha ya makampuni yote yaliyosajiliwa Tanzania na kufanya
upekuzi wa majina ili kutambua iwapo jina la biashara analotaka kusajili
limeshasajiliwa au la, kabla ya kutuma maombi ya kusajili.
Aidha fomu zote za usajili zinapatikana katika tovuti hiyo
ya BRELA pia wameweka katiba mfano inayojulikana kwa lugha ya kiingereza ‘Memorandum
and article of association’ ambapo mteja anaweza kuichukua na kutengeneza
katiba yake ya kusajili kampuni bila gharama yoyote.
BRELA ilianzishwa na kuzinduliwa rasmi Desemba 9, 1999 chini
ya wizara ya viwanda na biashara kwa sheria ya wakala za Serikali namba 30 ya
mwaka 1997. Ambapo majukumu yake makuu ni kusajili makampuni; kusajili majina
ya biashara; alama za bisahra na huduma; kutoa hataza-Uvumbuzi kwa muda maalum
(Patents of inventions) na kutoa leseni za viwanda na kusajili viwanda.
Boniphace Nyabweta (IDN)
10 Julai, 2013
DAR ES SALAAM, TANZAN