Wanajeshi saba Watanzania wauawa Dafur
Dar
es Salaam. Wanajeshi saba wa Tanzania, ambao ni miongoni mwa kikosi cha
Umoja wa Mataifa, cha kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini
Sudan, wanadaiwa kuwa wameuawa.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kwamba wanajeshi hao wa
Tanzania, wamekufa kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi
wanaopigana na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, miili yao wanajeshi hao bado ipo nchini Sudan ikisubiri taratibu za kusafirishwa kuletwa nchini.
Hii
ni mara ya kwanza kuripotiwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Tanzania
wanaolinda amani katika nchi mbalimbali kufa kwa wakati mmoja.
Agosti mwaka jana wanajeshi watatu wa Tanzania huko Darfur waliripotiwa kuuawa kwenye tukio kama hilo.
Msemaji
wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , Kanali Kapambala
Mgawe alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu vifo vya wanajeshi wa
Tanzania huko Darfur, alisema kuwa naye amesikia, lakini hana taarifa
rasmi kwa mujibu wa taratibu za kiofisi.
Hii
ni mara ya pili kwa wanajeshi wa Tanzania kuuawa katika Jimbo la
Darfur, ambapo Agosti mwaka jana, Kanali Mgawe alinukuliwa na vyombo
vya habari akithibitisha kutokea kwa vifo vya askari watatu ambao gari
lao lilizolewa na maji walipokuwa wakivuka mto uliokuwa umefurika maji.
Kanali
Mgawe aliwataja askari hao kuwa ni Sajini Julius Chacha, Sajini Anthony
Daniel na Koplo Yusuph Said na kwamba askari wengine walinusurika baada
ya kuogolea.
Tanzania
ina askari 850 kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani
jimbo la Darfur, ambao ni sehemu ya askari 1,081 wa kulinda amani
katika jimbo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Tanzania wametawanywa kwenye miji ya Khor Abeche na Muhajeria kusini mwa Darfur.
Aprili
mwaka huu Tanzania ilipeleka wanajeshi wa kulinda amani katika Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupambana na kikundi cha waasi wa nchi
hiyo M23 kinachopigana kuiangusha serikali ya DRC.
Majeshi
ya Tanzania yalipelekwa kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Tanzania inaungana na nchi za Afrika Kusini na Malawi kukamilisha
kikosi cha wanajeshi 3,000. Tanzania imepeleka wanajeshi 850.
ASANTE KWA KUTEMELEA BLOG YETU
ASANTE KWA KUTEMELEA BLOG YETU