Ponda anga kwa anga
Mwanachi
Kwa ufupi
- Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.
Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu mashtaka yanayomkabili.
Ponda jana alianza kwa kufikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi wa Kisutu asubuhi na kufutiwa mashtaka ya uchochezi
yaliyokuwa yakimkabili baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14, mwaka
huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili,
baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na
nia ya kuendelea kumshtaki.
Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.
Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi
na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya Wakili
Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, baada ya kufutiwa mashtaka hayo,
aliendelea kushikiliwa na kisha akachukuliwa na kupelekwa Morogoro
ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.Kuwasili Moro
Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta ya polisi na
kutua kwenye Uwanja wa Gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na
alipakiwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine
matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama
ukiwajumuisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa
upelelezi, Usalama wa Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha
shughuli za kazi katika Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa
muda.
Baada ya kufika mahakamani saa tano asubuhi,
magari yalisimama kwa takriban dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza
kwenye Mahakama ya wazi ambayo tayari ilikuwa umejaa watu.
Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara
uleule ulimrejesha Uwanja wa Gofu saa sita mchana na kupandishwa kwenye
helikopta kurejea Dar es Salaam. Mahakamani Morogoro
Ponda alisafirishwa kwa helikopta ya polisi hadi
Morogoro na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi akiwa
chini ya ulinzi mkali.