ukubwa wa habari
03.05.2013
“Kila siku uhuru wa kuzungumza unakabiliwa na vitisho vipya. Kwa sababu wanasaidia kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika masuala ya umma, waandishi wa habari mara kwa mara wanakuwa shabaha ya kushambuliwa”, alisema katibu mkuu Ban na Irina Bakova mkurugenzi mkuu wa idara ya Umoja wa mataifa kwaajili ya masuala ya elimu, sayansi na utamaduni-UNESCO katika ujumbe wa pamoja kusheherekea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani inayoadhimishwa kila mwaka Mei 3.
“Wafanyakazi wengi wa vyombo vya habari wanataabika kutokana na kunyanyaswa, vitisho na ghasia. Wengi wanakabiliwa na hali ya kukamatwa kiholela na kuteswa, mara nyingi bila ya kupata msaada wa kisheria. Lazima tusimame imara kukabiliana na ukosefu wa usalama na ukosefu wa haki za sheria”, walisema Ban na Bakova.
UNESCO na washirika wote wa mashirika yote huru ya vyombo vya habari wanatoa wito wa kuwepo ulinzi bora kwa waandishi wa habari duniani kote. Inasema waandishi wa habari 121 waliuwawa duniani kote mwaka 2012 takribani mara mbili ya idadi kulingana na mwaka 2010 na mwaka 2011.