JWTZ kuchunguza mauaji ya wanajeshi
Dar es Salaam. Wakati Rais
Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban K-Moon,
wamelaani mauaji ya wanajeshi wa Tanzania Jimbo la Darfur, Sudan, Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeunda timu ya kuchunguza tukio hilo.
Wapiganaji saba kati ya 36 wa Tanzania waliokuwa
kwenye Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa, (Unamid), waliuawa
Jumamosi na wengine 19 kujeruhiwa.
Mashambulizi hayo yalitekelezwa karibu na kambi ya Manawashi eneo la Khor Abeche, mji wa Darfur Jimbo la Nyala.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema
Dar es Salaam jana kuwa timu ya wataalamu itakwenda Darfur kuchunguza
tukio hilo.
Tukio hilo limekuwa la kushtua, kwani miaka mitano
ya majeshi ya kulinda amani kuwa huko haijawahi kutokea mauaji makubwa
kiasi kile.
Kanali Mgawe alisema wanawasiliana na UN kufanya taratibu za kurudisha nyumbani miili ya wapiganaji hao.
Taarifa ya Unamid
Taarifa ya iliyotolewa jana na Msemaji wa Unamid,
Christopher Cycmanick, ilisema wanajeshi hao waliuawa walipokuwa
kwenye doria ya kawaida.
Cycmanick alisema walinzi hao wa amani
walishambuliwa kwa bunduki na silaha nzito za kivita umbali wa kilomita
25 kutoka katika kambi yao.
JK atuma salamu za pole
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Rais
Kikwete ameeleza kushtushwa na tukio la kushambuliwa na kuuawa
wapiganaji wa JWTZ Mji wa Darfur, Sudan.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano,
Ikulu, ilisema Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, familia na wapiganaji
wote.