Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe akionyesha kitabu chenye mkusanyiko wa matukio ya wanachama wake
kuumizwa na wengine kupoteza maisha kwa madai ya kupigwa na polisi, alipo
zungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana. Picha na Michael Jamson
Posted Jumatano,Julai10 2013 saa 12:10 PM
Kwa ufupi
- Lengo ni kuwalinda wanachama na viongozi wake, chadai hakina imani na polisi, Usalama wa Taifa wala JWTZ
- Uamuzi huo unatokana na kauli ya Waziri Mkuu Pinda aliyoitoa Juni 19, mwaka huu katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu Bungeni Mjini Dodoma alipoviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
SHARE THIS STORY
Dar es Salaam. Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitaanzisha kambi nchi nzima kwa
ajili ya kuwapa mafunzo maalumu walinzi wa chama hicho ‘Red Brigade’, ili
waweze kuwalinda viongozi na wanachama wake.
Kimesema kimechukua hatua
hiyo kwa madai kwamba Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama
vimeshindwa kufanyia kazi malalamiko yake kuhusu mauaji, vitisho na matukio ya
kutisha wanayofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wake.
“Ni wajibu wa chama kutafuta
njia za kujilinda, hatulindwi na Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) wala Usalama wa Taifa, watu wetu wanapigwa na wanauawa hata tukienda
polisi hatupati haki yetu. Ni bora tuanzishe mafunzo na tujilinde wenyewe kwani
tukiendelea kupiga magoti na kulia tutakuwa wajinga,” alisema Mwenyekiti wa
chama hicho, Freeman Mbowe.
Aidha, chama hicho kimewataka
wabunge wake wote kushirikiana na wabunge wengine wenye mapenzi mema na nchi,
kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanzishe mchakato wa kupiga kura ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Uamuzi huo unatokana na kauli
ya Waziri Mkuu Pinda aliyoitoa Juni 19, mwaka huu katika Kipindi cha Maswali ya
Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu Bungeni Mjini Dodoma alipoviagiza vyombo
vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati
wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akisoma maazimio ya Kikao cha
Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kilichofanyika Dar es Salaam Julai 6 na 7,
Mbowe alisema wanaanzisha mafunzo hayo ili kukabiliana na fujo zinazofanywa na
walinzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ‘Green Guards’ ambao alidai katika kambi
zao wamepewa mafunzo ya kushambulia raia, hasa wanachama wa Chadema.
“Ili kukabiliana na fujo
zinazofanywa na vijana wa CCM ‘Green Guards’, sisi tuna kikosi cha ‘Red
Brigade’ ambacho ni kikosi kilichoundwa kwa mujibu wa katiba ya chama kwa ajili
ya kulinda mali za chama, labda kimekuwa legelege au kimezidi upole ndiyo maana
tunapigwa sana,” Mbowe alisema na kuongeza:
“Tutafanya mafunzo maalumu ya
vijana wetu nchi nzima, tutawafundisha namna ya kujilinda, tutaweka kambi kama CCM wanavyoweka kambi kufundisha vijana wao namna ya
kushambulia. Hatuwezi kuendelea kuwa mbuzi wa kafara.”
Viongozi wa CCM
hawakupatikana jana kuzungumzia kambi hizo zilizotajwa na Chadema kwani simu za
Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye ziliita bila ya kupokewa.
Alisema kambi ya chama hicho
itakuwa maalumu kwa ajili ya kuwafundisha vijana ukakamavu na jinsi ya
kujilinda.
Msajili wa Vyama vya Siasa,
John Tendwa hakupatikana jana kuzungumzia hatua hiyo ya Chadema kwani simu yake
ya mkononi ilikuwa haipatikani.
Katika maelezo yake, Mbowe
alisema viongozi wa chama hicho wamekuwa wakionewa katika matukio mbalimbali na
kudai kwamba hata wanapokwenda polisi kutoa taarifa hukamatwa na kushtakiwa.
Alisema katika mwelekeo huo, zaidi ya makada 2000 wa chama hicho
wameshafunguliwa kesi katika Mahakama mbalimbali nchini.